Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega
Na MWANDISHI WETU
Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amekabidhi Boti za kisasa 14 za uvuvi zilizotolewa
na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.2
kwa ajili ya wavuvi mkoani wa Tanga kwa lengo la kuboresha shughuli zao.
Waziri Ulega, amekabidhi boti hizo katika hafla fupi iliyofanyika mkoani Tanga Novemba 5, mwaka huu.
Akikabidhi boti hizo, Mhe. Ulega alisema Rais Samia amedhamiria kuboresha maisha ya wavuvi na ndio maana anatoa pesa nyingi kwa ajili ya kuziwezesha sekta za uzalishaji ikiwemo sekta ya uvuvi ziweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zikiwemo za uvuvi zinazidi kunufaisha Taifa na Watanzania kwa ujumla.
"Ndugu Wananchi,
siku ya leo katika mkoa wa Tanga tunakabidhi boti 14 zenye thamani ya takriban
Shilingi Bilioni 1.2 zenye ukubwa tofauti tofauti wa mita 7.06, 10, 12 na 14
ambazo zitagawiwa katika Halmashauri ya Pangani (6), Mkinga (4), Muheza (3) na
Tanga Jiji (1) ambapo zitanufaisha moja kwa moja wananchi 225, wakiwemo
wanaume 159 na wanawake 66," amesema Mhe. Ulega
Aliongeza kwa kusema kuwa mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya boti 160 zenye thamani ya shilingi Bilioni 11.5 zitatolewa kwa wanufaika nchi nzima huku zikitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa takriban watu 4,296 wakiwemo wavuvi mmoja mmoja, vikundi na vyama vya ushirika.
Aidha, Waziri Ulega alitumia fursa hiyo pia kukemea vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea huku akisisitiza kuwa boti hizo zilizokabidhiwa leo, ni mahsusi kwa ajili ya uvuvi endelevu tu na si vinginevyo, na kwamba, Serikali haitosita kuchukua hatua za kisheria ikigundua wavuvi wanajihusisha na uvuvi haramu au usafirishaji wa mazao haramu ya uvuvi.
0 Comments