Blog Post

MGOGORO WA WATUMISHI WAFUKUTA TAFIRI

 


Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Nchini (TAFIRI)

Na IBRAHIM KADILO

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvu Nchini (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirie, amemkingia kifua Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu na Utawala, Bi Joan Ndibalema ambaye anadaiwa kukiuka madili ya utumishi wa umma.

Akizungumza na blog hii kwa njia ya simu Dkt. Kimirie alikiri kuwa Bi Joan Ndibalema ni Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu na Utawala wa taasisi hiyo.

“Kama kuna mtu anayesema hana barua ya uteuzi wake kuwa mkuu wa idara ya utumishi ningetamani anioneshe mimi ndio mkuu natunza mafaili ya watumishi wote, itakuwa ni serikali ya ajabu kuruhusu mtu kama huyo kukaa kipindi chote hicho bila kuwa na barua inayomruhusu kushika wadhifa huo,” alisema Dkt Kimirie.

Dkt. Kimirie alitoa ufafanuzi huo kufuatia kuwepo kwa nakala za barua mbalimbali ambazo blog hii imezipata zikionesha kuwa Bi. Ndibalema analalamikiwa kwenye uongozi kuwa anakwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa barua hizo, Joan Ndibalema alitakiwa kutoa maelezo ya kiutendaji kwa kutokufika kazini bila kuwa na likizo ama ruhusa ya mwajiri, lakini pia aliandikiwa barua kwenda kwenye bodi ya wakurugenzi akilalamikiwa kufanya shambulio la aibu kwa maneno machafu kwa viongozi wake wa juu baadhi ya watumishi wenzake.

Bi Ndibalema anadaiwa kutokuwa na mahusiano mazuri na viongozi wake na amekuwa akitumia lugha chafu na kupelekea kufikishwakwenye bodi ya wakurungezi ya TAFIRI kwa barua iliyoandikwa tarehe 14 Septemba mwaka huu.

Pia, Ndibalema anapata stahiki zote kama Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu na Utawala wakati inadaiwa hana barua ya utumishi inayomruhusu kushika nafasi hiyo kwani kimsingi yenye ni ofisa mkuu.

Aidha, Bi. Ndibalema amekuwa hafiki kazini bila kuwa na likizo wala ruhusu ya mwajiri mara kwa mara kutokana na kuwa karibu sana mkurugenzi mkuu Dkt. Kimirie.

Pia, Bi. Ndibalema anadaiwa amekuwa akikaimu madaraka ya mkurugenzi wakati yeye sio mkuu wa idara.

Akijibu madai hayo, Dkt. Kimirie alisema kuwa kuna vitu vingine asilazimishwe kuvipa muhuri kwa kuhalalisha ugomvi wa watu wengine kuwa ni wa taasisi yake.

Dkt. Kimirie alisema kuwa hakuna mtumishi makao makuu ya taasisi hiyo ambaye hastahili kushika wadhifa wake na Joan Ndibalema anawezaje kaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu wakati yuko mkurugenzi wa idara ya utafiti na machapisho.

Akizungumzia madai yalioelekezwa kwake ya kutumia madaraka yake na fedha za taasisi hiyo vibaya, Dkt. Kimirie alisema kuwa tuhuma hizo hazina mashiko wala ukweli wowote.

Alisema kuhusu watumishi ambao hawajalipwa stahiki zao za uhamisho, hiyo ni changamoto hata yeye imemkumba alipohamishwa kutoka kigoma tarehe 20 Novemba 2019 hajalipwa stahiki zake za uhamisho.

Akijibu madai kuwa amekuwa akitumia fedha za taasisi kusafiri mara kwa mara mikoani na anasaini fedha za wiki na anakaa siku mbili anarudi ofisini, Dkt. Kimirie alisema madai hayo hayana ukweli kwani hawezi kuitwa Dodoma kwa shughuli za kiserikali kwa wiki mbili akakaa siku mbili na kurudi kwa nia ya kujinufaisha kwa kutumia fedha za taasisi vibaya.

“Niliwahi kupewa pesa ya kwenda Dodoma pesa ile sikuitumia nikarudi na kuikatia lisiti ofisini, yule anayesema nakwenda nakaa siku mbii narudi anafikiri mimi ni mjinga, ukitaka kufuatilia vizuri nenda tume ya maadili ya viongozi ambao nimekuwa nikijaza fomu zao halafu waulize” alisema Dkt. Kimirie

Aidha, Dkt. Kimirie amekiri kuwepo kwa mgogoro ndani ya taasisi hiyo kwa watumishi wake  na kusema kuwa hiyo ni hali ya kawaida wanapokuwepo watu na kumtaka mwandishi wa habari hizi kutotumika kama sehemu ya mgogoro wa watu binafsi na kuihusisha taasisi.

Alisema kuwa taasisi yake inawatumishi 145 migogoro haiwezi kukosa kwani kila mtu ana  familia yake na anapokuja ofisi wanatofautina hivyo hali kama hiyo ikichukuliwa kama mgogoro wa taasisi ni jambo la kumshangaza.

Alipopigiwa simu kujibu taarifa hizi, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu na Utawala Bi. Joan Ndibalema hakuweza kujibu lolote, alijibu kwa mkato na kumtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na viongozi wake wa juu.

Blog hii inaendelea kuwatafuta wakurugenzi wa bodi ya TAFIRI na viongozi wa Tume ya Maadili ya Watumishi wa Umma ambao hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu