Blog Post

Ujenzi wa Uwanja Msoga utainua michezo Pwani



Na Omar Mbarak  

NCHI yetu imepiga hatua kubwa sana katika michezo. Tukiendelea kusema kwamba bado tuko nyuma tutakuwa tunajidanganya wenyewe. 

Ni kweli kuna baadhi ya michezo imedorora sana, lakini kama nchi hatujapoteza yote. Kuna baadhi ya maeneo tunaweza kutembea vifua mbele na kusema kama nchi tumeweza.

Ndiyo, mchezo wa soka umeibeba sana Tanzania. Kufanya vema kwa timu za Simba na Yanga kimataifa, kufanya vema kwa timu zetu wa wanawake za mchezo huo, kumeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazokwenda mbele kwenye soka.

Lakini kama nchi, tuna malengo makubwa zaidi. Tumesikia kwa mfano, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kwamba ikifika mwaka 2027, Tanzania iwe mmoja wa wenyeji wa michuano mikubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa kushirikiana na jirani zetu, Kenya na Uganda.

Huu ni mkakati wa ukanda huu. Kama tumeshindwa kufuzu kwenye AFCON kwa kupitia mfumo wa kawaida, tunaweza kuwa washiriki kwa kuandaa mashindano.

Lakini ili kuwa wenyewe si kazi rahisi. Tunahitaji kuwa na viwanja vya kutosha, tunahitaji kuwa na miundombinu sahihi pamoja na huduma zote zinazoweza kubeba wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

Tunaweza kuwa na hoteli za kisasa, huduma zote muhimu ambazo Tanzania tunazo, lakini kama hatuna viwanja vya kisasa vinavyotosheleza kila hatua hatuwezi kufanya lolote.

Taarifa kwamba Mbunge wa Chalinze na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba wilaya ya Chalinze inakuwa na uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kubeba watu elfu 10, ni moja ya taarifa njema kabisa.

Juzi nimeona Kikwete ameandika kwenye Twitter yake akisema Ujenzi wa Uwanja huo wa Mpira Miguu wa Riadha wenye uwezo wa kuingiza watazamaji Elfu Kumi unaojengwa Msoga, Chalinze unaendelea na kwamba kazi inayofanywa sasa ni kuweka sawa jamvi la uwanja huo.

Hii maana yake ni kwamba kama ujenzi huo ukikamilika, utakuwa moja ya viwanja vizuri hapa nchini, utakuwa sehemu ya viwanja ambavyo vinaweza kutumika kwenye AFCON mwaka 2027, hata kama sio kwa ajili ya mechi, lakini hata kwa mazoezi kwa ajili ya baadhi ya timu.

Uwanja huu unaweza kuwa na sifa za ziada kama pia kasi ya Maendeleo ya Wilaya ya Chalinze itazidi kuwa kubwa.

Wanaopita na kufika Chalinze mara kwa mara wanajua kwamba Wilaya inakwenda kasi, kuna maendeleo ambayo yanaonekana kwa macho.

Si ajabu ikifika mwaka huo wa 2027, Chalinze ikawa na Hoteli kubwa za kisasa ambazo zinaweza kubeba baadhi ya timu kwa ajili ya kuweka kambi huko.

Lakini pia uwanja huo unaweza kusaidia mkoa wa Pwani wenyewe ambao hauna uwanja wa kisasa, kupata morari ya kuwa na timu hata ya Ligi Kuu baada ya ile ya Ruvu Shooting kushuka daraja.

Mkoa unapokuwa na viwanja bora, inaongeza hamasa kwa vijana kuchangamkia michezo, na kwasababu michezo imekuwa ajira muhimu sana, tutegemee kuona mabadiliko makubwa kwenye wilaya ya Chalinze na mkoa wa Pwani kwa ujumla.


Post a Comment

0 Comments

Close Menu