Na Moses Mwakibolwa,
Mto Nyakasangwe unaopatikana katika eneo la Boko, Manispaa ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji uangalizi mkubwa HASA tukizingatia kipindi cha mvua kubwa. Hali ya mabadiliko ya tabianchi na uwezekano wa vipindi vya mvua kubwa ulio tangazwa hivi karibuni na watabiri wa Hali ya hewa hivyo kuongeza umuhimu wa jamii na mamlaka kuchukua hatua za mapema katika kulinda mto na maeneo yanayouzunguka.
Mvua kubwa zinapotokea, kiwango cha maji katika mto kinaweza kuongezeka kwa haraka. Endapo mkondo wa maji utakuwa umezibwa na taka, udongo au mimea isiyodhibitiwa, kuna hatari ya maji kutiririka nje ya mkondo wake na kusababisha mafuriko katika maeneo ya jirani.
TAKA NI TISHIO KUBWA
Tatizo la utupaji wa taka ovyo linaweza kuongeza hatari wakati wa mvua. Mifuko ya plastiki, chupa, mabaki ya ujenzi na taka nyingine zinapoingia kwenye mto zinaweza kusafirishwa na maji na kukwama katika maeneo yenye vizuizi.
Mto unapozibwa, uwezo wake wa kupitisha maji hupungua. Hali hiyo inaweza kuongeza kasi ya maji na kusababisha mmomonyoko wa kingo, uharibifu wa mazingira na hatari kwa makazi na miundombinu iliyopo karibu na mto.
KINGO ZA MTO ZINAHITAJI KULINDWA
Mmomonyoko wa kingo ni changamoto nyingine inayoweza kuongezeka wakati wa mvua kubwa. Maji yenye nguvu yanaweza kuondoa udongo wa kingo na kufanya maeneo hayo kuwa hatarishi.
Hatua za kurejesha uoto wa asili, kupanda miti na mimea inayosaidia kushikilia udongo, pamoja na kuzuia shughuli zinazoharibu kingo za mto, ni muhimu katika kupunguza athari hizi.
NI WAKATI WA KUCHUKUA HATUA, SI KUSUBIRI MAAFA
Wadau wa mazingira, Serikali za mitaa, wananchi, taasisi binafsi na mashirika ya mazingira wanapaswa kushirikiana katika kuandaa mpango wa kulinda Mto Nyakasangwe.
Hatua hizo zinaweza kujumuisha kufanya usafi wa mto na maeneo yake, kuondoa vizuizi kwenye mkondo wa maji, kuelimisha wananchi kuhusu utupaji sahihi wa taka, kupanda miti na kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa maeneo hatarishi.
Vijana wanaweza pia kushirikishwa kupitia programu za Taka Zero (Zero Waste), ambapo taka zinazoweza kurejelewa hukusanywa na kutenganishwa badala ya kutupwa kwenye mito na mifereji.
JAMII YA BOKO INA NAFASI KUBWA
Ulinzi wa Mto Nyakasangwe hauwezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayouzunguka. Kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha taka hazitupwi kwenye mto, mifereji au maeneo yanayoweza kusababisha taka kusombwa na maji.
Shule, vikundi vya vijana, wanawake, viongozi wa mitaa, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali wanaweza kuwa sehemu ya kampeni ya pamoja ya “Linda Mto Nyakasangwe”.
WITO KWA WADAU
Mto Nyakasangwe ni sehemu ya mfumo wa mazingira wa eneo la Boko na unahitaji kulindwa kabla ya madhara makubwa kutokea.
Ni muhimu mamlaka na wadau kufanya tathmini ya hali ya mto, kubaini maeneo yenye hatari ya mafuriko na mmomonyoko, na kuweka mpango wa hatua za haraka kabla na wakati wa msimu wa mvua kubwa.
Tusisubiri mto ufanye maafa ndipo tukumbuke kuutunza.
Kulinda Mto Nyakasangwe ni kulinda mazingira, makazi, afya na usalama wa jamii ya Boko.
WITO: TAKA ZERO – LINDA MTO NYAKASANGWE
Jamii inaweza kugeuza changamoto ya taka kuwa fursa kwa kutenganisha taka, kuchakata zinazoweza kurejelewa, kutengeneza mboji kutokana na taka za kikaboni na kuhakikisha taka haziishii kwenye mito.






0 Comments