Na Omary Mbaraka
*Tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021, Serikali imechukua hatua kubwa za makusudi kutatua na kupunguza migogoro ya ardhi nchini. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya migogoro 18,005 ya ardhi imetatuliwa kwa njia mbalimbali, ikiwemo njia za kiutawala. Migogoro hiyo ilikuwa imekumba vijiji 981 na mitaa 23 kote nchini.*
Kupitia mikakati madhubuti kama vile uamuzi wa Baraza la Ardhi la Taifa (BLM), kuanzishwa kwa Kliniki za Ardhi, upimaji wa ardhi, pamoja na uboreshaji wa mifumo ya usajili na utoaji wa hati miliki, Serikali imeleta mabadiliko makubwa yanayoonekana kwa macho.
Katika hatua nyingine ya mafanikio, Serikali chini ya Rais Samia imefanikiwa kusajili vyeti vya ardhi kwa vijiji 766, na hivyo kufanya jumla ya vijiji 10,987 kati ya vijiji 12,333 vilivyopo nchini kuwa na vyeti halali vya ardhi.
Aidha, hadi kufikia mwaka 2024, mafanikio mengine makubwa ni pamoja na kusajili hati miliki 356,642, kutoa hati za sehemu ya jengo 1,282, pamoja na kushughulikia miamala na nyaraka za hatimiliki 444,447. Pia kumekuwa na ongezeko la usajili wa hatimiliki kutoka 67,331 hadi 99,366 nchini kote.
Hatua hizi zimeongeza imani ya wananchi kwa Serikali na kuimarisha usalama wa miliki za ardhi, jambo ambalo ni muhimu katika kukuza uchumi na kuvutia uwekezaji nchini.
0 Comments