MAWAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, wameanza kwa kishindo utekelezaji wa majukumu yao mapya.
Mawaziri hao ambao ni miongoni mwa wateule walioapishwa juzi baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni, walianza kutekeleza majukumu yao mara moja baada ya kutoka katika hafla ya uapisho, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ndejembi baada ya kutoka Ikulu, alikwenda moja kwa moja katika ofisi za wizara hiyo, Dar es Salaam na kuzungumza na viongozi na watumishi huku akitoa maagizo kadhaa kuhusu utendaji kazi.
Ridhiwani kwa upande wake, baada ya kuapishwa alikwenda ofisi za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kukutana na menejimenti chini ya Mkurugenzi Mkuu, Masha Mshomba.
Hakuna kilichowekwa bayana kati ya Ridhiwani ambaye kabla ya wadhifa huo alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na viongozi wa mfuko huo.
Hata alipotafutwa kwa njia ya simu alisema: “Hatukuwa na mazungumzo rasmi zaidi ya kusalimiana. Nitaanza kazi rasmi Jumatatu (kesho),|” alisema Ridhiwani.
Baada ya kuwaapisha viongozi hao na wengine, Rais Samia pamoja na mambo mengine, alimwagiza Ridhiwani kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii isitetereke kwa kuwa inahifadhi fedha za wafanyakazi kwa ajili ya mustakabali wao baada ya kumaliza ajira.
Rais Samia alisema katika mifuko hiyo kuna miradi mingi iliyoanzishwa kwa kutumia fedha za wafanyakazi lakini haijaleta matokeo Chanya, hivyo ahakikishe kunakuwa na usimamizi makini.
Ndejembi, ambaye alikuwa akishikilia mikoba aliyopewa Ridhiwani, baada ya kufika katika ofisi za Ardhi, Dar es Salaam, alitoa maagizo mbalimbali kwa watumishi ikiwamo kuongeza uadilifu na kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yao sambamba na kuongeza kasi katika utendaji kazi.
Alibainisha kuwa suala la ardhi ni gumu na linahitaji watumishi kuwa makini huku akisisitiza kuwa ni lazima watende haki huku wakizingatia sheria, kanuni na miongozo inayowaoongoza katika utendaji kazi.
Pamoja na msisitizo huo, alisema ataendeleza mazuri yote yaliyofanywa na mtangulizi wake, Jerry Silaa ambaye amekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, zikiwamo Kliniki za Ardhi ili kuleta ufanisi wa wizara.
‘’Sikuja kutangua torati. Yote aliyoyaanzisha mtanguluzi wangu ikiwamo kliniki za ardhi zitaendelea,” alisema na kusisitiza kuimarishwa kwa mifumo ndani ya wizara ili migogoro ya ardhi isiendelee kujitokeza.
Jana, Ndejembi alifanya kikao na menejimenti ya wizara hiyo katika makao makuu ya wizara yaliyoko Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma na kutaka menejimenti na watumishi kuondoa urasimu na kutoa hati milki za ardhi kwa wakati.
“Tuondoe urasimu. Kama mtu ana nyaraka zote zinazohitajika, tuwape hati zao na tukumbuke sisi ni watoa huduma kwa wananchi na ni wizara wezeshi. Hati zitolewe kwa wakati na hati zilizo tayari wananchi wajulishwe waje wachukue.
Tuzidi kufanya kazi vizuri na mifumo yetu ya kiwizara kuanzia wilaya, mikoa na wizara ifanye kazi vizuri. Ni vizuri tusimamie haki ya wananchi na mifumo ifanye kazi yake kutoa haki,” alisema.
0 Comments