Na Mohammed Ussi
SERIKALI imeombwa kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za kusambaza Gesi nchini kutokana na Malalamiko ya baadhi ya Wananchi kwamba kuna udanganyifu mkubwa katika mitungi hiyo.
Wakizungumza na Mwandishi wa Habari hizi, baadhi ya Wananchi hao wamesema Gesi wanayotumia kwa matumizi ya kawaida haifiki hata mwezi mmoja, wakati huko nyuma hali haikuwa hivyo.
"Huko nyuma Mimi nilikuwa natumia Gesi kwa hadi miezi miwili, lakini sasa hivi haifiki hata mwezi mmoja kwa matumizi yaleyale", amesema Mwananchi mmoja, Zawadi Hassan mkazi wa Keko Magurumbasi wilayani Temeke Jijini Dar es Salaam.
Mwingine aliyelalamika ni Helena Mweta, mkazi wa Buza pia Wilayani humo ambaye amesema pamoja na kubadilisha Wakala aliyekuwa anamuuzia Gesi, lakini bado ametumia Gesi kwa wiki tatu tu.
"Huu ni wizi mkubwa, hii mitungi haifiki hata kilo sita. Tunawaomba Ewura na Serikali kwa ujumla kuunda kikosi kazi cha kukagua mitungi ya Gesi, wataona uhalisia wa kile tunacholalamika", amesema.
Ameitaja kampuni moja (jina tunalihifadhi) kwamba imekuwa ikilalamikiwa zaidi kutokana na Gesi iliyoko kwenye mitungi yake kumalizika haraka zaidi.
"Hawa watu wanatuzishia Umasikini, haiwezekani kila baada ya wiki tatu ununue Gesi. Mimi nipo tayari kuwapa ushirikiano Serikali", amesema.
0 Comments