Na Mwandishi wetu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya utoaji wa tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani
Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kukuza sekta ya viwanda nchini kwa kuongeza ufanisi, uwekezaji, ajira na mchango wake katika pato la Taifa. Mikakati hiyo inalenga kuchakata malighafi zinazozalishwa nchini na kuongeza thamani yake.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya 19 ya utoaji wa tuzo kwa wazalishaji bora wa Viwanda kwa Mwaka, iliyofanyika Septemba 2, 2026 katika ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wazalishaji wa saruji nchini, kuhakikisha wanatafuta suluhu ya haraka ili kurejesha bei ya kawaida ya saruji kwa wananchi. Amesema maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wanaweza kununua mfuko wa saruji kwa gharama nafuu, hivyo ni lazima kuoanisha uzalishaji wa malighafi zote zinazochangia katika uzalishaji wa saruji ili bidhaa hiyo ipatikane kwa urahisi.
Makamu wa Rais ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wafanyabishaara wote wanaojihusisha na biashara haramu za uingizaji bidhaa bandia ambazo hukwepa kodi na tozo mbalimbali stahiki ambapo, zinaathiri ukuaji wa viwanda, kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali pamoja na kupunguza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.
Amewataka wazalishaji wa viwandani hapa nchini, kufanya jitihada za kuongeza uchakataji wa malighafi za ndani ya nchi kwa kuhakikisha wanaongeza thamani, hatua itakayosaidia katika kuongeza ajira kwa watanzania na ukuaji wa uchumi kwa kasi.
Makamu wa Rais amesema katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watanzania, sekta ya viwanda ina nafasi kubwa kwa kuwa ndiyo chimbuko la maendeleo ya haraka na ni muhimili mkuu katika uongezaji thamani wa malighafi zilizopo, utoaji ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya Serikali pamoja na fedha za kigeni. Pia, amesema sekta ya viwanda ni muhimu katika kuboresha sayansi na teknolojia na kuongeza uzalishaji, na hivyo kukuza ubunifu, uvumbuzi, uchumi, na kuondoa umasikini nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga, amesema Wizara hiyo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha lengo lake la kuendeleza sekta ya viwanda linafanikiwa. Amesema Sekta hiyo imeendelea kujiimarisha ili kuongeza nafasi katika mchango wa pato la Taifa na kuongeza ufanisi kwa lengo la ukuaji wa sekta hiyo muhimu.
Amesema tayari Wizara imekamilisha na itazindua Sera ya Maendeleo endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya jasiriamali ndogo na za kati ya mwaka 2003 Toleo la mwaka 2025 ikiwa na lengo la kwenda sambamba na Dira 2050 ambayo inategemea uendelevu wa Viwanda.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Hussein Suphian Ally ameipongeza Serikali kwa mafanikio mbalimbali yanayoendelea kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda nchini ikiwemo uwekezaji mkubwa unaofanywa katika miradi ya kimkakati ambayo imeendelea kuongeza ushindani katika sekta ya viwanda.
Katika hafla hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezawadia tuzo ya heshima kwa kutambua mchango wake katika uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na viwanda nchini.
Hafla hiyo imewakutanisha wazalishaji wakubwa, wakati na wadogo, wafanyabiashara pamoja na wadau wengine wa sekta ya viwanda na biashara, huku tuzo hizo zikiendelea kuwa jukwaa la kuhamasisha ubora, ubunifu, uwekezaji, matumizi ya teknolojia na uzalishaji endelevu nchini.



0 Comments