Na Casiana Mwanyika
NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula ametoa wito kwa wananchi kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali za Elimu na binafsi zinazoshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Elimu Kitaifa, mkoani Pwani ili kupata elimu na uelewa utakaosaidia maboresho ya Elimu nchini.
Dkt. Rwezimula ameyasema hayo akiwa katika banda la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Oktoba 11, 2023 ikiwa ni siku ya tatu ya Maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima Kitaifa yanayofanyika viwanja vya Maili moja, Kibahamkoani Pwani.
NACTVET imeshiriki Maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa duniani kote mwezi Septemba kila mwaka ambapo Tanzania mwaka huu inaadhimisha Wiki ya Elimu ya Watu Wazima kuanzia kuanzia Oktoba 9 - 13.
Lengo la Maadhimisho hayo ni kuwajengea uelewa wadau wote wa Elimu nchini kwa kutilia uzito juu ya nafasi ya Elimu ya Watu Wazima na kwamba inaendana na mazingira ya sasa, ambayo ni tofauti na zamani ambapo elimu hiyo iliyojikita zaidi kwenye Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
Mwelekeo wa sasa unakazia kisomo ni chenye manufaa ( Functional Literacy) kwani watu hufundishwa kusoma, kuandika na kuhesabu kuendana na kazi wanazozifanya ili kuwawezesha kufanya vitu tofauti kutokana na mahitaji ya sasa ya jamii yetu, mathalan; kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu huku walengwa wakijifunza ujuzi aina mbalimbali kama vile kutengeneza sabuni.
NACTVET wamekuwa wakishiriki maonesho hayo kama sehemu ya uelimishaji umma na kusogeza huduma za Baraza hilo karibu zaidi na wateja na wadau mbalimbali.
Kwa kupitia fursa hiyo wananchi wamepata nafasi ya kutatuliwa changamoto zao na kuelimishwa juu ya Majukumu ya NACTVET.
Baraza hilo ni chombo lilichoundwa kwa sheria ya Bunge sura Na.129 kutekeleza jukumu kubwa la kusimamia ubora katika utoaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Nchini.
0 Comments