Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dkt Adolf Rutayuga.
Na Mdoe Kiligo, MeCAP
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limetoa tahadhari kwa Wazazi na Wanafunzi wanaotarajia kujiunga na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
NACTVET ambacho ni chombo kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Sura ya 129, ili kusimamia na kuratibu utoaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, imesema kuna udanganyifu unaofanywa na baadhi ya Vyuo vinavyotoa Elimu ya Ufundi.
"Kati ya majukumu ya Baraza ni kusajili vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi na kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi vigezo na ubora kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Chini ya Sheria hii, vyuo vyote vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi vinapaswa kuzingatia taratibu za usajili. Taratibu hizi ni pamoja kufundisha kozi zilizopata ithibati na udahili wa wanafunzi kuzingatia vigezo vilivyoainishwa katika mitaala na miongozo mbalimbali. Udahili wa wanafunzi huzingatia sifa na vigezo vilivyowekwa katika mitaala iliyopitishwa na Baraza.", imesema taarifa ya Ofisi ya Katibu Mtendaji wa NACTVET juzi na kuongeza:
"Kama mnavyofahamu, hiki ni kipindi ambacho wanafunzi waliodalihiwa katika vyuo mbalimlali vya kati wanapaswa kuanza masomo.
Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya vyuo kutumia mbinu za udanganyifu kwa kuwadahili wanafunzi katika vyuo visivyosajiliwa au kufundisha kozi zisizotambulika na mamlaka yoyote ya udhibiti ubora".
Taarifa hiyo imeongeza kuwepo kwa Kozi zitolewazo na vyuo visiyokuwa na ithibati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi au mamlaka zinatotambulika kisheria hazitambuliki.
NACTVET imesema kuna changamoto ya baadhi ya vyuo ambavyo havijasajiliwa na au vilivyosajiliwa kuendesha mafunzo kinyume na taratibu, kanuni na sheria.
Baraza hilo linaloongozwa na Katibu Mtendaji wake Dkt Adolf Rutayuga limesema ukiukaji huo ni pamoja na ama kuendesha mafunzo bila usajili au kutangaza na kudahili wanafunzi katika kozi zisizotambulika.
"Hivi karibuni mmeshuhudia kupitia vyombo vya habari malalamiko ya wanafunzi 17 wa Chuo cha Afya cha DECOHAS, cha Dodoma, ambao walidahiliwa kwa udanganyifu katika kozi ya Afya ya Jamii (Community Health). Kozi hii ilifutwa tangu mwaka 2019, na Baraza kuwataarifu wadau kuwa kozi hiyo haitafundishwa tena. Hata hivyo, kinyume na utaratibu, Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha DECOHAS kwa makusudi, kiliwadahili wanafunzi hao 17 kusoma kozi iliyofutwa na mamlaka.
Chuo hicho kinaruhusiwa kutoa Kozi tatu (3) tu, za fani ya Afya zikiwemo Utabibu (Clinical Medicine), Uuguzi na Ukunga (Nursing and Midwifery) na Famasia (Pharmaceutical Sciences)."
Baraza hilo limesema baada ya kupokea taarifa ya kufukuzwa chuo wanafunzi hao 17 baada ya kulalamikia udanganyifu huo, limechukua hatua kadhaa dhidi ya chuo cha DECOHAS, ikiwemo kukiagiza chuo hicho kuwarudishia wanafunzi wote walioathirika na kadhia hiyo gharama ambazo ni ada walizotumia wakati wa masomo hayo.
Aidha, Baraza limechukua jukumu la kuwapangia wanafunzi hao masomo katika vyuo vya Serikali kulingana na sifa za ufaulu wao.
"Hivyo, Baraza linachukua fursa hii kuwashauri wazazi na wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo mbalilmbali kwa mwaka wa masomo 2023/2024 kuzingatia, pamoja na mengine kuhakiki vyuo na kozi walizochagua kusoma kwenye tovuti ya Baraza.
" Tafadhali, wazazi na wanafunzi wajiridhishe kuhusu usajili wa vyuo na ithibati ya kozi zake ili kuepuka udanganyifu wa baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu. Taarifa zote za vyuo na kozi zilizosajiliwa zinapatikana katika tovuti ya NACTVET ambayo ni www.nactvet.go.tz kwa kuangalia Mwongozo wa Udahili (Admission Guidebook) au kwa kutupigia simu" imesema taarifa hiyo.
0 Comments